Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Friday, March 18, 2016

Namna Unavyoweza Kuondoa Mawazo Hasi Katika Maisha Yako.

No comments :
Mwanadamu ni kiumbe ambaye amepewa uwezo mkubwa sana wa kufikiri. Na katika uwezo huo huwa mara nyingi anakuwa ana mawazo chanya na mawazo hasi. Mimi na wewe kwa namna moja au nyingine huwa ni watu wa kutumia mawazo haya, yawe chanya au hasi lakini tunakuwa nayo.
Kila siku tunavyoishi huwa tunakuwa na mawazo mengi sana kwani akili ya mwanadamu huwaza kila dakika. Hebu fikiria sasa hivi na jaribu kuandika mawazo yako ambayo unafikiria kwa takribani kila siku. Mangapi kati ya mawazo hayo huwa ni hasi? Naweza kusema kwamba asilimia kubwa ya watu wengi, mawazo yao ni hasi. Naamini utaniunga mkono katika hili.
Je, unajua kwamba mawazo yetu yana nguvu kubwa sana ya ajabu na pia yana uwezo kwa asilimia kubwa sana kubadili maisha yetu. Akili inaweza ikawa ni kitu kigumu sana kukimiliki na kukitawala kama usipokuwa makini. Lakini unapoongeza umakini katika kuitumia akili yako, itakusaidia kufanikisha mipango yako mingi iliyokwama.
Siku zote ukitaka kuwa mchezaji mzuri ni lazima ufanye mazoezi sana. Hivyo basi hata ukitaka ubongo wako kufikiri chanya ni lazima uufanyishe ubongo wako mazoezi mengi sana ya kutosha. Hiyo itasaidia ubongo wako kufikiri kutoka hasi na kuanza kufikiri chanya.

FANYA TAHAJUDI AU SALA KUTOA MAWAZO HASI.
Kwanini ni muhimu sana kuondoa mawazo hasi? Hiyo yote ni kwa sababu mawazo hasi ni kizuizi kikubwa cha kufikia mafanikio yako. Kama ukitaka kuacha kufikiria mawazo hasi kuna njia ambazo unaweza kuzitumia na ukaweza kufikia malengo yako.
Kwanza, soma vitu vya kukufanikisha.
Dunia ya leo ina kelele nyingi sana ambazo ni hasi na hazina maana wala msaada sana kwako. Ili uweze kutoka huko ni muhimu kwako kujilisha au kusoma vitu vya kukufanikisha. Hapa unaweza ukasoma vitabu, majarida ya mafanikio au hata ukahudhuria semina.
Usikubali kukaa kienyeji enyeji, poteza fedha zako kwenye kununua au kusoma vitabu mitandaoni ambavyo vinaweza kukusaidia kukuongeza uwezo wako wa kufikiri chanya.  Kwa kujijengea mawazo chanya itakupelekea wewe mwenyewe kufikia ndoto zako.
Pili, fanya tahajudi(Sala).
Wakati mwingine mawazo hasi yanakuwa sio rahisi sana kuondoka mpaka ufanye tahajudi au sala. Hili ni tendo ambalo unaweza ukawa unalifanya kila siku. ‘Kumediteti’ hakuhitaji nguvu kubwa sana, inaweza ikawa rahisi sana na ukafanikiwa kuondoa mawazo hasi.
Unapoanza kutaka kufanya tahajudi au ‘meditation’ funga macho yako, wakati huo huo unavuta pumzi taratibu huku ukiwa umetulia kimya ukitafakari hali unayotaka ikutokee. Unapofanya hivi kwa muda utajikuta unapata majibu na kufanikisha malengio kwa sababu unachukua muda kuuongoza ubongo wako.
Tatu, andika mawazo mazuri.
Baada ya kuhisi kuwa una mawazo chanya yanaanza kuleta mwamko wa mafanikio, unaweza ukawa na kitabu cha kumbukumbu zako( Diary)  na ukaamua kuyaingiza yale mawazo unayayona ni mazuri na yanaweza kuleta mabadiliko mara moja.
Zoezi hili la kuandika mawazo mazuri litakusaidia sana kupunguza mawazo hasi katika akili yako na kwa kuanzia hapo utaupa uwezo ubongo wako kuwaza mawazo chanya na yenye mafanikio kwa upande wako.
Nne, usikate tamaa.
Hata inapotokea unaona mawazo yako hasi kama hayatoki na bado yapo, jifunze kutokukata tamaa mapema. Amini mawazo yako hayo yataanza kutoka polepole. Kitu kikubwa uwe una nia ya kuamini kwamba ni lazima utakuwa una mawazo chanya muda sio mrefu.
Ni matumaini yangu ya kwamba utatumia njia hizo katika kukusaidia kukupa mawazo chanya yenye manufaa kwako na kitaifa pia. Pia usisahau kumwomba Mungu akusaidie.

Shukrani za pekee zimwendee Nickson Tarimo kwa kutushirikisha makala haya, kumbuka endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa kujifunza zaidi.

No comments :

Post a Comment