Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Monday, July 10, 2017

Jifunze Namna Ya Kupiga Hatua Za Kimafanikio Kila Wakati.

No comments :
Moja kati ya siri kubwa iliyopo katika mafaikio yako ni vile utakavyoamua wewe kuchukua hatua kwa kile kidogo au kikubwa ambacho unakifahamu. Huwezi kusema unataka kufanikiwa wakati maarifa uliyonayo, ambayo ndiyo nguzo ya mafanikio hayo unayaweka pembeni.
Hata hivyo watu wengi wanaamini ya kwamba siri kubwa ya kufanikiwa kwao ipo katika kuendelea kujifunza vitu vipya pekee, jambo hili kwa macho mawili huenda likawa ni sawa, ila kwa jicho la tatu kufanya hivyo pekee yake haitoshi.
Nimesema haitoshi kwa sababu watu wengi wana maarifa mengi sana na ya  kutosha katika halmashauri zao za vichwa, ila wao tatizo linakuja kuweza kubadilisha maarifa hayo kuwa bidhaa au huduma ambazo zitawaingizia  wao kipato.

Zijue hatua za mafanikio yako.
Na ukweli ambao hauna kificho ni kwamba  kitu pekee kitakacho kufanikisha kuweza kufika mbali zaidi kimafanikio si wingi wa maarifa ya mafanikio unayoyapata kila siku. Mafanikio yako utayapata kwa wewe kuamua kuyatumia maarifa hayo tena kwa uhakika.
Lakini pia jambo la msingi ambalo huna budi kujiuliza kila wakati ni hili, Jiulize, tokea uanze kujifunza juu ya mafanikio, umechukua hatua kiasi gani? Au umebakia kuwa ni mtu wa kushangilia na kuwaacha wengine wachukue hatua za kimafanikio? Mara baada ya kujiuliza naomba usinipe majibu, kwani ukweli wa majibu hayo unao wewe.
Lakini kama umepata majibu ya kwamba hakuna jambo lolote lenye heri ambalo umelifanya tangu uanze kujifunza mambo ya mafanikio ni vyema kuanzia sasa kuamua kuwa mtu wa vitendo zaidi kuliko maneno.
Kwani yale maneno ambayo umekuwa ukijfariji kila wakati ya kwamba nitafanya kesho, ni maneno yenye faraja na yenye kuleta msisimko mzuri maishani. Ila ukweli ni kwamba  maneno hayo hayo pasipo kuweka katika matendo ni maneno yajengayo majuto maishani, hivyo ni vyema kuwa ni  mtu wa kusema kwa matendo kuliko maneno. Kwani upo usemi usamao ya kwamba matendo ni maneno halisi.
Hivyo kabla sijaweka nukta  siku ya leo naomba niseme ya kwamba kwa kila kitu ambacho unajifunza kila siku ni heri kuchukua hatua zaidi, kwani ni heri kuwa na hamsini nzima kuliko kuwa na mia mbovu. Na ukitaka kufanikiwa zaidi maishani ni vyema kuacha maneno na uweke vitendo.
Imeandaliwa na mtandao huu wa dira ya mafanikio,
Imani Ngwangwalu & Benson Chonya,

No comments :

Post a Comment