Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Friday, July 21, 2017

Watu Wenye Hasira Na Kiu Kubwa Ya Mafanikio Wanafanya Mambo Haya Kwa Utofauti Sana.

No comments :
Wapo watu ambao ndani mwao wameamua kwa dhati kufanya mabadiliko katika maisha yao. Watu hawa wana kiu, hasira na hamasa kubwa ya kufanya kila kinachowezekana ili kuweza kufanikisha ndoto zao za kimaisha.
Watu hawa juhudi zao nyingi huzielekeza kwa kufanya mambo kwa utofauti hali ambayo huwaletea mafanikio. Inawezekana leo nitakuwa mbaya kwako, kama sitakwambia watu hawa wanafanya mambo yapi kwa utofauti na yanayowapa mafanikio.
Ni wakati sasa wa mimi na wewe kwenda pamoja katika makala yetu ya leo kujifunza kwa pamoja mambo ambayo watu wenye hasira na kiu ya mafanikio huyafanya tofauti;-
1. Wanaongozwa sana na neno HAPANA.
Watu wenye hasira na kiu ya mafanikio, kila wakati wanapoambiwa kitu ni watu wakusema sana HAPANA. Wanafanya hivi ili kufatilia ndoto zao kwa ukaribu na kuachana na kukubali kila kitu ambacho kinaweza  kuwapoteza.
Watu hawa wanajua pia kwa kusema hapana kwanza  hata kama kitu hicho walichoambiwa wakagundua kina faida kwao, ni rahisi kugeuza na kukubali pia. Kusema HAPANA ni jambo ambalo haliogopwi  na watu wenye hasira ya mafanikio.
2. Kuamka asubuhi na mapema.
Naomba nikupe tu ukweli mmoja, ukiachana na watu maskini, sijawahi kukutana na mtu mwenye mafanikio makubwa ambaye kuamka kwake asubuhi ni kwa kuchelewa. Watu wengi wenye mafanikio wanaamka mapema kabla jua halijatoka.
Asubuhi ni muda mzuri unaowawezesha kupanga mipango ya siku husika kwa uhakika na kufatilia mambo kwa ukaribu wakati wengine bado wamelala. Kuamka mapema mi kitu ambacho wengi hawapendi, kwa watu wenye hasira na mafanikio hupenda sana muda huo.
3. Kujituma sana.
Kati ya kitu ambacho watu wenye hasira na kiu ya mafanikio wanakifanya sana pia ni kujituma kwa nguvu zote. Wanajua bila kujituma itakuwa ni kazi bure tu, hakuna mafanikio yatakayojengwa.
Hujitahidi kufanya kazi kwa muda mrefu sana kuliko watu wengine ili kuleta matokeo chanya. Si ajabu kukuta usiku wa manane wakifanya kazi zao ili kufanikisha ndoto zao. Kujituma na kwenda hatua ya ziada ni kitu ambacho kinafanywa na watu hawa.
4. Wanaongozwa na roho ya ung’ang’anizi.
Watu wenye kiu ya mafanikio pia wanajaribu sana mambo mengi na kuhakikisha kila wanalolifanya linafanikiwa. Wakianzisha jambo si rahisi sana kuliachilia njiani. Hung’ang'ana na kuhakikisha mpaka kuona kutaka kuleta matokeo.
Kwa kifupi, watu wenye hasira na mafanikio ni wabishi wa mafanikio yao. Hawakubali kirahisi kushindwa. Wapo tayari kufanya mara elfu moja, ilimradi tu kuona wanafanikiwa. Hiki ni kitu kimojawapo wanachokifanya kwa utofauti pia.
5. Si walevu wa mitandao ya kijamii.
Mitandao ya kijamii ni mizuri kutusaidia kupashana habari , nafikiri hilo unalijua vizuri sana. lakini kwa watu wenye kiu na hasira ya mafanikio wanaamini sana kwamba mitandao ya kijamii imewekwa kwa ajili ya kuwapotezea au kuwaibia muda wao.
Hivyo kwa kulijua hilo wanaitumia mitandao ya kijamii kwa hesabu sana na kwa muda maalumu. Tofauti na watu wengine wanavyofanya, wao wana muda maalumu kuingia kwenye mitandao hiyo ya kijamii, lakini sio kuingia hovyo hovyo tu.
6. Kutokujali sana mambo ya wengine.
Kitu kikubwa kilicho ndani ya watu wenye kiu ya mafanikio na kinachowapelekea wafanye mambo yao kwa utofauti na kuleta mafanikio, ni kule pia kutokujali mambo ya watu wengine. Hawajali sana fulani anafanya  kitu gani.
Kila wakati ni watu ambao wanajihusisha sana na ndoto zao na kuangalia ni wapi pa kuboresha hadi kuleta matokeo. Hawajali wanakoselewa vipi na nani. Huamua kusonga mbele bila kujali vitu kama hivyo na hatimaye hufanikiwa.
7. Wasikilizaji wazuri wa mambo na kuchukua hatua.
Kila wakati watu wenye nia  ya kufikia mafanikio, ni wasikilizaji wazuri sana kwa wengine wanasema nini. Ni watu ambao wanajua kusema sana kunapoteza mafanikio, hivyo huamua kusikiliza na kuweka kumbukumbu za kimaandihi vile vitu ambavyo vinawasaidia.
Ndio maana ukiwafatilia wengi ni watu ambao wapo makini na si waongeaji sana. Huamua kujifunza kupitia maisha ya wengine, huchukua vitu vya msingi vinavyoweza kuwasaidia kufanikiwa.
Kila la kheri katika kufikia mafanikio makubwa na endelea kujifunza kupitia DIRA YA MAFANIKIO kila siku.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali,
Blog, dirayamafanikio.blogspot.com
Mawasiliano; +255 767 048 035, +255 713 048 035,
Email; dirayamafanikio@gmail.com

No comments :

Post a Comment