Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Sunday, July 23, 2017

KITABU; The Success System That Never Fails (Mfumo Wa Mafanikio Ambao Haushindwi)

No comments :

Kwenye  kitabu hiki mwandishi W. Clement Stone anaeleza upo mfumo katika maisha , ambapo ukiutumia mfumo huo vizuri, utayafanya maisha yako yasiwe ya kushindwa kamwe, bali yawe ya mafanikio siku zote.
Katika mfumo huo mwandishi ameongelea mfumo usioshindwa katika maisha jinsi ulivyokuwa wa muhimu katika maisha yako. Na mfumo huo umebebwa sana na mambo makubwa matatu ambayo ni;-
Hatua/vitendo (Action)
Hapa inakubidi kuchukua vitendo kwa kitu unachotakiwa kufanya. Unatakiwa kuchukua vitendo bila kujali kitu. Kitu unachokifanya kama umeamua kukifanya, kifanye. Acha kupoteza muda chochote unachokiamini, hebu kifanye bila woga.
Kujua namna ya kufanya (Know-how)
Kuchukua hatua kwenye jambo lolote yenyewe haitoshi peke yake, unatakiwa sasa kujua namna ya kufanya kitu hicho tena. Unatakiwa kujua namna ya kufanya katika hali ambayo itakupa matokeo sahihi.
Maarifa (Knowledge)
Maarifa ni kitu cha msingi katika kufanikisha jambo lolote lile. Lazima uwe umeiva kwa maarifa ya kutosha ili yakusaidie kufanya mambo yako kwa usanifu wa hali juu na kukupa mafanikio. Ukikosa maarifa ya msingi kwa jambo lolote utashindwa.
Hayo ndiyo mambo matatu ya msingi sana ambayo mwandishi ameyasititiza na kuyatilia mkazo karibu katika kitabu chake chote. Mambo mengine ya kujifunza kwenye kitabu hiki ni kama haya yafuatayo;-
1. Maamuzi mazuri katika maisha yanaendana na kuchukua hatua. Kama huchukui hatua, halafu ukasema eti una maamuzi mazuri, basi elewa unajidanganya na  maamuzi hayo hayana maana yoyote kwako kwa sababu hayawezi kukusaidia.
2. Kama umeamua kufanya kitu fulani, iwe ni biashara , masomo au kitu chochote ambacho kipo kwenye malengo yako, usirudi nyuma hadi umefanikisha kitu hicho. Haijalishi njiani umekutana na changamoto nyingi kiasi gani, pambana mpaka upate kile kitu ambacho ulikuwa umelenga kukifanikisha.
3. Unaweza ukaongeza uwezo mkubwa wa kufanikiwa ikiwa utatumia kanuni za mafanikio na kuzifanyia kazi kila siku. Unaweza pia ukapunguza hali ya kushindwa sana kwenye maisha yako, ikiwa kama utaendelea kutumia kanuni hizo hizo za mafanikio. Kama utafanya kinyume na hapo jiandae na anguko kubwa la maisha yako.
4. Mafanikio yanakuja kwa wale wote wanaojaribu hiki au kile mara kwa mara bila kujali wanashindwa kwa kiasi gani. Huwezi kuwa mshindi kama umekaa tu. Jaribu kwa jinsi unavyoweza ili kujenga mafanikio yako.
5. Kila wakati hakikisha unayatawala mazingira yako na sio mazingira yakutawale. Epuka kila hali iwe mazingira au watu wakutawale. Hakikisha unatawala mazingira yako vizuri ili yakupe nguvu ya kushinda.
7. Kufikiri peke yake hakuwezi kukafanya wewe ukashinda uoga ulionao. Kitu kitakachoweza kukufanya ukashinda uoga ulionao ni zile hatua unazochukua. Hatua au vitendo ni dawa pekee ya kuondoa hofu au woga wowote ule kwako.
8. Kama hujiwekei akiba yoyote, elewa kabisa ndani yako umekosa mbegu ya mafanikio. Wanaojiwekea akiba hata kama ni pesa kidogo sana, hiyo inawasaidia kuweza kukuza mbengu ya mafanikio iliyo ndani mwao. Angalia watu wengi ambao hawaweki akiba, maisha yao sio mazuri na kufanikiwa inakuwa ni ngumu.
9. Moja ya sifa kubwa ya mafanikio unayotakiwa kuwa nayo na kuiendeleza ni TABIA zako ulizonazo. Ukiwa na tabia sahihi, uwe na uhakika zitakuongoza hadi kuweza kufikia mafanikio yako.
10. Ukishakijua vizuri kile unachokitaka kwenye maisha yako, tafuta maarifa na mbinu za kukichimba kitu hicho ndani, nje mpaka ukielewe vizuri. Kukijua vizuri kitu hicho ndani, nje itakupa wewe uwezo wa kukifanya kwa ufasaha sana na kupata matokeo chanya.
11. Nguvu ya kuendelea kufanya jambo lolote itazidi kuchochewa ndani yako kama moto, ikiwa ndani yako pia una hasira, imani ya kufanikiwa na pengine maumivu ya kuumizwa na wengine. Kama ndani yako unavitu hivyo, itachochea nguvu kubwa iliyoko ndani yako ya kufanikiwa na utafanya kila linawezekana kuhakikisha unafanikiwa.
12. Unapokuwa una hamu na hamasa ya kufikia malengo yako, ni lazima kutafuta njia na kila aina ya maarifa yatakayokusaidia kufikia malengo yako. Maarifa hayo utayapata kutoka kwa watu ambao tayari wameshafanikisha hicho unachokitaka au hata kwenye vitabu mbalimbali vya kimafanikio.
13. Ili ukijue vizuri hicho unachotaka kukifanya ni lazima uchuke hatua. Huwezi kukijua kitu hicho kwa kusoma peke yake ni muhimu kuchukua hatua zitakazo kupa uzoefu ambao uzoefu huo utapelekea wewe kujua namna ya kufanya kwa ubora wa hali ya juu.
14. Kama kuna jambo ambalo umelianzisha hata kama linakuletea utata endelea kulifanya. Ikiwa kama utasimama inachukua muda mrefu tena kulianza jambo hilo na kuwa kwenye mwendo sahihi kuliko ungeendelea na safari. Siri ya kuendelea ipo kwenye kufanya sasa hicho unachotaka kukifanya. Acha kujisemea kuwa utafanya kesho au lini, fanya sasa.
15. Siku zote mafanikio ya mtu yanaanzia kwenye akili yake. Unachotakiwa kufanya ni kuangalia fursa zinazokuzunguka au changamoto zinazoizunguka jamii yako na kisha baada ya hapo tafutia majibu yake na utafanikiwa.
.16. Maadili bora ni msingi mkubwa wa mafanikio yoyote. Kushindwa kwingi kunaanza pale mtu anapokosa maadili na kujiingiza kwenye tabia za hovyo kama ulevi, zinaa na hata wizi. Mafanikio hayajengwi kwenye misingi kama hiyo hata siku moja.
Chukua hatua kila siku kujifunza haya muhimu uliyojifunza kwenye kitabu hiki.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali,
Blog, dirayamafanikio.blogspot.com
Mawasiliano; +255 767 048 035, +255 713 048 035,
Email; dirayamafanikio@gmail.com

No comments :

Post a Comment