Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Wednesday, July 5, 2017

Misingi Minne (4) Ya Kufikia Mafanikio Makubwa Katika Kila Eneo La Maisha Yako.

No comments :
Kila mtu ana ndoto na maono ya kufikia mafanikio makubwa maishani mwake. Binafsi, nimekutana na watu wengi sana ambao ukiwasikiliza hisia zao wanataka kufikia mafanikio makubwa kwenye shughuli wanazozifanya..
Lakini pamoja na ndoto hizo, cha kushangaza, bado watu wengi ambao wanataka kufikia mafanikio makubwa, wamekuwa wakiishi kwa matumaini sana pasipo kuchukua hatua au kufanya mambo  yatakayowafikisha huko.
Watu hao wamekuwa wakisahau kwamba kufikia mafanikio makubwa ni safari ambayo sio rahisi na hiyo haitoshi, ni safari ambayo inahitaji kujitoa sana na kujua misingi yake vyema, bila ya hivyo hakuna mafanikio tena.
Kupitia makala haya ya leo, nataka twende pamoja kujua misingi minne ya lazima itakayokusaidia kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako. Katika misingi hiyo, mimi na wewe tunatakiwa kuijua vizuri ili kufikia mafanikio makubwa.
1. Amua kuwa mwenyewe.
Kila mtu anataka mafanikio makubwa, lakini si kila mtu anataka kupita kwenye njia inayoleta mafanikio makubwa. Njia ambayo inaweza ikakufanya ukawa na mafanikio makubwa ni wewe kuamua kuwa mwenyewe.
Unajiuliza kivipi? Sikiliza, wakati wengine wanafanya kazi saa 8 kwa siku, wewe fanya kazi saa kumi na mbili. Wakati wengine wanaamka saa kumi na mbili asubuhi, wewe amka saa kumi na moja alfajiri na kuanza kutekeleza majukumu yako.

Ijue vyema misingi ya kufikia mafanikio makubwa.
Unafanya yote hayo si kwa kutaka sifa, bali unatengeneza mafanikio yako na njia hiyo ya kupata mafanikio makubwa wengi hawataki kupita huko. Ikiwa hutaki kufanya hivyo utaambulia patupu, mafanikio makubwa hutaweza kuyapata.
Kama ingekuwa rahisi kupata mafanikio makubwa kama wengi wanavyotaka na kusema, basi kila mtu angekuwa nayo hayo mafanikio, lakini inataka kazi, kuwekeza juhudi na kulipa gharama ambazo wengine hawataki kulipa, ukifanya hivyo, hapo mafanikio makubwa utayanasa.
2. Tengeneza imani zinazokuongoza kwenye mafanikio yako.
Linapokuja suala mafanikio makubwa, wewe binafsi unaamini kitu gani? unaamini ili upate mafanikio makubwa ni lazima utumie uchawi au ni kitu gani ambacho unachoamini? Imani yako hapa ni muhimu sana katika kukuongoza kufanikiwa.
Wakati mwingine unatakiwa ujenge imani tofauti, utumie kanuni kinyume na wengi wanavyofikiri mafanikio yanataka yawe. Amua kufanikiwa katika eneo ambalo hata wengine hawaoni kama kweli utaweza kufanikiwa.
3. Tengeneza maono makubwa.
Kinachotofautisha kati ya watu ambao wamefanikiwa na wale ambao hawajafanikiwa si kitu kingine bali ni maono. Watu waliofanikiwa wanaongozwa na ndoto au maono makubwa ya kimafanikio tofauti na ambao hawajafanikiwa.
Unapotengeneza maono yako makubwa na ukaamua kuyafatilia kila siku, ni wazi ipo siku utafikia ndoto zako. Hakuna kinachoweza kushindikana katika kufikia mafanikio makubwa kama kweli una maono makubwa na yaliyowazi.
4. Fanya mambo yako kwa ubora.
Mafanikio makubwa yanajengwa kwa kufanya vitu kwa ubora na umakini wa hali ya juu. Kama unafikiri mafanikio yanakuja hivihivi tu yaani kwa kulipua mambo uwe na uhakika huwezi kufanikiwa.
Kila wakati kaa chini na anza kufikiri jinsi ya kufanya mambo yako kwa ubora, yaani ‘how to commit to excellence’. Siri ya mafanikio makubwa unayoyataka ndivyo inavyotakiwa kufanyiwa kazi na kuleta matokeo.
Kwa kufanya mambo hayo kikamilifu basi utakuwa ni moja ya watu ambao utaweza kufikia mafanikiio makubwa.
Kila la kheri katika kufikia mafanikio makubwa na endelea kutembelea dirayamafanikio.blogspot.com kila siku kujifunza.
Kama unataka kufanya biashara au upo kwenye biashara na unataka wazo bora kabisa la kuboresha biashara yako, usisite kuwasiliana nasi mara moja kwa 0713 04 80 35 au tutumie email dirayamafanikio@gmail.com kwa msaada zaidi.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali,
Blog, dirayamafanikio.blogspot.com
Mawasiliano; +255 767 048 035, +255 713 048 035,

Email; dirayamafanikio@gmail.com

No comments :

Post a Comment