google-site-verification: googleabbfd1327a3af7a3.html

Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Kujifunza zaidi juu ya maisha na mafanikio, nakualika kwenye kundi la whats app kujifunza kwa kina. Tututumie ujumbe kwa njia ya whats app kwenda 0687449428 kupata utaratibu wa kujiunga.

Aug 26, 2017

Kama Utafanya Mambo Haya, Utakumbukwa Wakati Wote Duniani.

No comments :
Yupo mtu mmoja ambaye katika wakati wake aliwahi kusema ‘haijalishi utaishi maisha ya kifahari na kitajiri kiasi gani, ila utakumbukwa tu kwa jinsi ulivyogusa maisha ya watu na wala sio pesa zako’. Ukiangalia kauli hiyo, huo ndio ukweli.
Katika maisha tunayoishi ni kweli vipo vitu ambavyo ukivifanya, ni rahisi kuacha alama ambazo alama hizo zitakumbukwa na vizazi karibu vyote hata ukiwa umekufa. Ni alama hizi hizi ambazo ingetakiwa kila mtu aziache.
Kitu cha kujiuliza je, unaweza ukaacha alama za kukumbukwa na watu duniani, au siku ukifa basi ndio historia imeishia hapo? Majibu unayo wewe, lakini najua kuna watu ambao unawajua historia zao ni kubwa sana mpaka leo, ingawa wamekufa siku nyingi.

Fanya mambo yatakayakufanya ukumbukwe wakati wote.
Labda nikuulize unafikiri walifanya nini watu hao? au unafikiri wanakumbukwa kwa bahati mbaya. Kiuhalisia, yapo mambo ambayo walifanya ndio yanasababisha. Kwa kufanya mambo hayo, hata wewe ukiwa nayo, ni lazima utaacha alama duniani.
Kupitia makala haya ya leo, nataka tuangalie mambo ya msingi ambayo ukiyaendeleza kwa usahihi na ukawa nayo basi elewa kabisa siku ukija kuiacha dunia hii utakumbukwa kwa muda mrefu na hautayeyuka kama moshi.
Jambo la kwanza, mchango ulionao.
Hauwezi kukumbukwa au ukaacha alama duniani kama huna mchango mkubwa kwa jamii unayoishi. Je, maisha yako unayoishi sasa yana mchango kwa wengine? Maisha yako yanaleta unafuu kwa wengine? Je, unaishi kwa kusaidia wengine?
Unatakiwa ukae na kujiuliza maswali mengi na kuangalia kila eneo je, una msaada kwa wanaokuzunguka? Kugusa maisha ya wengine hata kama hauna pesa unaweza kufanya hilo. Ukiweza kugusa maisha ya wengine, utaweza kukumbukwa sana duniani.
Kama unafikiri natania, waangalie watu wote ambao wameacha historia kubwa duniani, waligusa maisha ya watu, ukiangalia kuanzia wapigania uhuru waligusa maisha ya watu wengi ndio maana nwanakumbukwa mpaka leo.
Lakini leo hii ukiwa unataka kuishi kwa ubinafsi, ukabaki wewe kama wewe, nikwambie tu siku ukitoka kwenye hii dunia ndio kwa heri, hauna alama au kumbukumbu ambayo utakuwa umeiacha ya maana, utakufa wewe kama wewe.
Jambo la pili, mahusiano.
Mbali na mchango ulionao je, mahusiano na watu wako wa karibu yakoje? Je, una mahusiano ya kubomoa au ya kujenga. Unapokuwa na mahusiano bora, elewa kabisa unajenga msingi mmojawapo wa kuacha alama duniani.
Faida ya kuwa na mahusiano bora inakusaidia wewe kuwa kiongozi bora wa maisha yako na wengine pia. Hata kama hujachaguliwa kwa kura lakini jinsi unavyowaongoza watu hiyo inatafsiriwa moja kwa moja wewe ni kiongozi kwa maisha ya watu.
Unataka kujenga jina na unataka kuacha alama za uhakika duniani, anza kujenga mahusiano  bora na watu wengine. Jenga mahusiano na watoto, jenga mahusiano na watu wazima, jenga mahusia na kila mtu, utafanikiwa.
Jambo la tatu, tabia.
Mbali na mchango ulionao kwa wengine jambo lingine ambalo linaweza likakupelekea ukaacha alama katika maisha yako ni tabia. Hapa kitu cha kuangalia tabia ulizonazo ni zipi, je zinawafurahisha wengine au kila mtu anakereka na tabia zako?
Haiwezekani ukawa na tabia mbaya na za hovyo halafu wakati huohuo ukawa ni mtu ambaye unategemea ukaacha kumbukumbu kwa wengine. Unapokuwa na tabia njema kama za kusaidia wengine ni wazi utakumbukwa.
Wengi ambao tabia zao ni mbaya sana, huishia kukumbukwa kwa muda tu lakini baada ya hapo husahaulika sana. Hivyo, unaona pia tabia ni moja ya kitu ambacho kinaweza kikamfanya mtu akaacha alama duniani.
Kwa kuhitimisha, ukiangalia kwa kina hayo ndiyo mambo ya msingi yanayopelekea moja kwa moja kwa yeyote kuweza kuacha alama duniani ikiwa atayafanya. Ni jukumu letu sote kuweza kufanyia kazi mambo haya ili tuwe na maisha ya msaada kwa wengine.
Nakutakia mafanikio mema na endelea kutembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza kila siku maisha na mafanikio.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali,
Mawasiliano; +255 767 048 035, +255 713 048 035,

No comments :

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.