Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Wednesday, August 2, 2017

Kama Utajiuliza Maswali Haya, Mafanikio Kwako Hayakwepeki Tena.

No comments :
Kuna watu ambao wanafikiri kwamba, kama watafanya kazi kwa bidii sana na kuianza siku yao mapema na kukamilisha majukumu yao muhimu ya siku, basi hapo ndipo kila kitu kimekwisha, mafanikio ni lazima watayapata.
Uhalisia katika kufikia mafanikio unatambua yote hayo ni muhimu sana tena sana ila yatafanya kazi kama pia utakuwa umejijengea tabia ya kujiuliliza maswali yatakayokupa upenyo ama njia sahihi ya kuweza kufanikiwa.
Kama utashindwa kujiuliza maswali ya msingi ambayo tunakwenda kuyangalia katika makala haya, usishangae ukashindwa kufanikiwa. Unaweza kutoa kila kitu ikiwa pamoja na juhudi, nidhamu lakini unashangaa mambo hayaendi kama unavyotaka yawe.
Nafikiri kuna wakati umeshawahi kujiuliza ni kitu gani unachokosa au ni wapi unapokosea hadi usifanikiwe kwa viwango vikubwa uvitakavyo? Haya ni maswali pengine yamekuumiza sana kichwa na hujui ni nini shida.
Kama ilivyo ada ya DIRA YA MAFANIKIO tunakushirikisha mafanikio, kupitia makala haya, sasa naomba twende pamoja kujifunza na nikuonyeshe maswali ambayo unatakiwa ujiulize mara kwa mara ili kujenga mafanikio yako.
1. Ni kitu gani ninachokiweza kwa uhakika?
Katika maisha yako haujazaliwa kufanya kila kitu. Vipo vitu vichache au kitu ambacho utakifanya dunia nzima inaweza ikabaki ikakushangaa. Sasa moja ya kitu ambacho unatakiwa kujiuliza sana je, unaweza kufanya nini kwa uhakika?
Usiniambie hujui, na kama unasema hujui, hiyo yote inaonyesha ni kwa jinsi gani hapo ulivyo mvivu wa kufikiri. Kila mtu duniani kipo kitu ambacho anakiweza hata kama ni kidogo sana, lakini anakiweza.
Kuna anayeweza kufuma vitambaa, kuna anayeweza kusuka, kuna anayeweza kuimba na kuna anayeweza kuandika. Sasa jiulize wewe unaweza nini yaani ukipewa kitu hicho basi, shida za watu zimefika mwisho. Hili ni swali la kujiuliza sana ili kufanikiwa.

Jiulize maswali muhimu ya kukupa mafanikio.
2. Ninataka kuwa nani maishani mwangu?
Piga picha ya maisha yako kama vile wewe ndiye‘staring’ wa picha la maisha yako. Jiulize unataka kuwa nani, hapa unatakiwa kujiuliza kila siku.  Unapojiuliza swali hili mara kwa mara unashangaa litakupa msukumo mkubwa wa kutenda zaidi.
Kama utakuwa unaishi tu, na hata hujui unataka kuwa nani, si rahisi kuweka juhudi kubwa zitakazoweza kukutoa hapo ulipo. Ukishajijua wewe maisha yako siyo ya umaskini, utafanya kila linalowezekana utoke hapo.
Washindi katika maisha hujiuliza sana swali hili. Swali hili linakupa utambuzi wa kujijua wewe ni nani na kujikuta hata mambo ya kujinga ambayo ulikuwa unataka kuyafanya huwezi kuyafanya. Ukijiuliza pia swali hili mafanikio huwezi kuyakwepa kwako.
3.  Ni akina nani wanaonizunguka?
Wataalamu wa mambo ya mafanikio wanasema wewe ni matokeoo ya watu watano wanaokuzunguka. Sasa ili ufanikiwe unatakiwa ujue unazungukwa na akina nani?, jiulize tena je, watu hao wanakusaidia kufanikiwa?.
Kama marafiki zako ni watu chanya, maskini na ambao hawana mchango hata kidogo kwenye maisha yao huwezi kufanikiwa. Sikwambii uwakimbie rafiki zako lakini huo ndio uhalisia ulivyo. Unatakiwa kuzungukwa na marafiki makini ili kufanikiwa.
Ikiwa hitaji lako la kwanza kubwa ni mafanikio, achana na watu ambao hawakusaidii. Kila siku jiulize kama ni urafiki nilionao, unanisaidia kunifikisha kwenye mafanikio?  Timu inayokuzunguka ni muhimu sana kukupa mafanikio yako ya kimaisha.
Mpaka kufika hapa unaona ili kufanikiwa kwenye maisha mbali na juhudi nyingi ambazo tunatakiwa kuziweka kila siku, pia moja ya kitu cha msingi ambacho tunatakiwa kuwa nacho au ni kutambua maswali yatakayokupa mafanikio.
Nikutakie siku njema na kila la kheri katika kufikia mafanikio makubwa, lakini kumbuka endele kutembelea dirayamafnikio.blogspot.com kila siku.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali,
Mawasiliano; +255 767 048 035, +255 713 048 035,
Email; dirayamafanikio@gmail.com

No comments :

Post a Comment