Badili maisha yako sasa kwa kuwa na fikra sahihi.

Tuesday, August 1, 2017

Miaka Kumi (10) Ijayo Kuanzia Leo, Utakuwa Upo Wapi Kimafanikio?

No comments :
Kati ya kitu ambacho unatakiwa kukifanya sana kwenye maisha yako wakati upo kwenye safari yako ya mafanikio ni kufanya tathmini ya wapi ulipo, wapi ulipotoka na wapi unapokwenda. Tathmini ni muhimu sana kwako.
Nakwambia hivi kwa sababu, bila kufanya tathmini za mara kwa mara ni rahisi kujikuta ukiwa unazunguka pale pale pasipo kuelewa kwa nini upo hapo. Kampuni na biashara makini zinaelewa umuhimu wa kufanya tathmini mara kwa mara.
Biashara au kampuni hizi nyingi hufanya tathmini ya siku, wiki na hata mwezi kuangalia maendeleo yapo vipi. Kama hiyo iko hivyo kwenye taasisi na hata kwenye  maisha yako unatakiwa kujenga utaratibu wa kujiwekea tathmini.
Hautakiwi uishi tu kama mnyama, unatakiwa uwe na utaratibu wa wiki au mwezi kujipa tathmini ya maisha yako yalipofika. Hiyo inakusaidia kukupa nguvu na hamasa ya kusonga mbele, hasa baada ya kuona pale ulipokuwa umekosea.

Piga tathmini ya maisha yako.
Hautaweza kufafanikiwa sana, kama utakuwa upo upo tu na hakuna tathmini unayoichukua. Utaratibu wa kujiwekea tathmini ni muhimu kwenye maisha yako kuliko unavyofikiri ili uweze kupiga hatua.
Na moja ya kitu ambacho unatakiwa kujiuliza je, baada ya muda fulani maisha yako yatakuwa wapi, baada ya miaka mitano maisha yako yatakuwa ya aina gani, baada ya miaka kumi maisha yako ya kimafanikio yatakuwaje?
Hautakiwi kuishia hapo tu, pia unatakiwa ujue kama ndio mwendo huo wa maisha yako ulionao sasa, je, mwendo huo utakufikisha wapi? Kama unaishi sasa bila kuwekeza jiulize baada  miaka kumi ambapo pengine mwili wako maisha utakuwa umechoka, ni nini kitatokea?
Ni rahisi sana kwa sasa kufurahia maisha yako, na kupoteza pesa zote unazozipata kizembe na kusahau kesho yako itakuwaje? Kuna wakati unakuja ambao kile unachokifanya leo utakuwa hauwezi tena kukifanya, kama leo utazembea hivyo nini kitaokea?
Najua pia kuna kitu ambacho unakitegemea kwa sasa kinakuingizia kipato, jiulize kama kitu hicho unacho sasa,  ni nini kitatokea ghafla kama kitu hicho kikaondolewa na ndicho ulichokuwa unakitegemea maisha yako yatakuwaje?
Kufanya tathmini kwenye maisha yako ni jambo la  muhimu sana ambalo unatakiwa uanze kulifanyia kazi ili uweze kufanikiwa. Kama matendo yako hayakupeleki kwenye mafanikio, elewa miaka kumi ijayo utakuwa na hali mbaya kiuchumi ukiendelea hivyo.
Anza kubadilika kwa kile unachokiingiza kwenye akili yako kila siku. Soma vitu vya kukusaidia na kaa na watu ambao ni chanya na kujenga mstakabali wa maisha yako kwenye miaka kumi ijayo.
Ikiwa leo utaishi kizembezembe, nikupe uhakika, andika maumivu hautaweza kusogea kimafanikio. Hatima ya maisha yako unayo wewe mwenyewe. Hilo unatakiwa ulijue vyema na kufanya vitu vitakavyookoa maisha yako siku za mbeleni.
Nikutakie siku njema na kila la kheri, fanyia kazi haya machache na endelea kutembelea dirayamafanikio.blogspot.com kila siku kwa ajili ya kujifunza na kuhamasika.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali,
Blog, dirayamafanikio.blogspot.com
Mawasiliano; +255 767 048 035, +255 713 048 035,
Email; dirayamafanikio@gmail.com


No comments :

Post a Comment